-->
logo

033 - Al-Ahzaab

الأَحْزاب
Al-Ahzaab: 33

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ


يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ اتَّقِ اللَّـهَ وَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَالْمُنَافِقِينَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١﴾
1. Ee Nabiy! Mche Allaah na wala usiwatii makafiri na wanafiki; hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.


وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿٢﴾
2. Na fuata yale ulofunuliwa Wahy kutoka kwa Rabb wako; hakika Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.


وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿٣﴾
3. Na tawakali kwa Allaah, na Anatosheleza Allaah kuwa ni Mdhamini.”


مَّا جَعَلَ اللَّـهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ ۚ وَمَا جَعَلَ أَزْوَاجَكُمُ اللَّائِي تُظَاهِرُونَ مِنْهُنَّ أُمَّهَاتِكُمْ ۚوَمَا جَعَلَ أَدْعِيَاءَكُمْ أَبْنَاءَكُمْ ۚ ذَٰلِكُمْ قَوْلُكُم بِأَفْوَاهِكُمْ ۖ وَاللَّـهُ يَقُولُ الْحَقَّ وَهُوَ يَهْدِي السَّبِيلَ ﴿٤﴾
4. Allaah Hakufanya mtu yeyote kuwa na nyoyo mbili kifuani mwake; na wala Hakufanya wake zenu ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu kuwa ni mama zenu; na wala Hakufanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni watoto wenu khasa. Hizi ni kauli zenu za vinywa vyenu tu. Na Allaah Anasema ya haki Naye Anaongoza njia (ya haki).


ادْعُوهُمْ لِآبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِندَ اللَّـهِ ۚ فَإِن لَّمْ تَعْلَمُوا آبَاءَهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَمَوَالِيكُمْ ۚوَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥﴾
5. Waiteni kwa (majina ya) baba zao, hivyo ndio uadilifu zaidi mbele ya Allaah. Na ikiwa hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na walio katika ulinzi wenu, na wala hakuna dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini isipokuwa katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu; na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuriaMwenye kurehemu.


النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ ۖ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ ۗ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ إِلَّا أَن تَفْعَلُوا إِلَىٰ أَوْلِيَائِكُم مَّعْرُوفًا ۚ كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا ﴿٦﴾
6. Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na wenye uhusiano wa damu wana haki zaidi (katika kurithiana) wao kwa wao katika hukumu ya Allaah kuliko (undugu wa) Waumini na Muhaajiriyna, isipokuwa mkiwafanyia wema marafiki wenu wa karibu. Hayo yamekwishaandikwa Kitabuni.


وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۖ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا ﴿٧﴾
7. Na pale Tulipochukua kutoka kwa Manabii fungamano yao na kutoka kwako, na kutoka kwa Nuwh, na Ibraahiym, na Muwsaa, na ‘Iysaa mwana wa Maryam; na Tukachukua kutoka kwao fungamano gumu.


لِّيَسْأَلَ الصَّادِقِينَ عَن صِدْقِهِمْ ۚ وَأَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿٨﴾
8. Ili Awaulize wakweli kuhusu ukweli wao; na Amewaandalia makafiri adhabu iumizayo.



يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَاءَتْكُمْ جُنُودٌ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا وَجُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا ۚ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا ﴿٩﴾
9. Enyi walioamini! Kumbukeni neema ya Allaah juu yenu, pale yalipokujieni majeshi Tukawapelekea upepo wa dhoruba na majeshi msiyoyaona (ya Malaika). Na Allaah daima ni Mwenye kuona myatendayo.   


إِذْ جَاءُوكُم مِّن فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّـهِ الظُّنُونَا ﴿١٠﴾
10. Walipokujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu, na macho yalipokodoka, na nyoyo zikafikia kooni na mkamdhania Allaah dhana nyingi.


هُنَالِكَ ابْتُلِيَ الْمُؤْمِنُونَ وَزُلْزِلُوا زِلْزَالًا شَدِيدًا ﴿١١﴾
11. Hapo ndipo Waumini walipojaribiwa na wakatetemeshwa tetemesho kali kabisa.



وَإِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ مَّا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ إِلَّا غُرُورًا ﴿١٢﴾
12. Na pale waliposema wanafiki na wale ambao nyoyoni mwao mna maradhi: “Allaah na Rasuli Wake Hawakutuahidi isipokuwa ni ghururi tu,”



وَإِذْ قَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْهُمْ يَا أَهْلَ يَثْرِبَ لَا مُقَامَ لَكُمْ فَارْجِعُوا ۚ وَيَسْتَأْذِنُ فَرِيقٌ مِّنْهُمُ النَّبِيَّ يَقُولُونَ إِنَّ بُيُوتَنَا عَوْرَةٌ وَمَا هِيَ بِعَوْرَةٍ ۖ إِن يُرِيدُونَ إِلَّا فِرَارًا ﴿١٣﴾
13. Na pale waliposema kundi miongoni mwao: “Enyi watu wa Yathrib!  Hamna uimara basi rudini (makwenu)!” Kundi miongoni mwao likamwomba idhini Nabiy, likasema: “Hakika nyumba zetu ziko tupu!” Na wala hazikuwa tupu! Hawakutaka ila kukimbia tu!



وَلَوْ دُخِلَتْ عَلَيْهِم مِّنْ أَقْطَارِهَا ثُمَّ سُئِلُوا الْفِتْنَةَ لَآتَوْهَا وَمَا تَلَبَّثُوا بِهَا إِلَّا يَسِيرًا ﴿١٤﴾
14. Na lau wangeliingiliwa kutoka pande zake zote (za mji), kisha wakatakwa fitnah (kuritadi) basi wangeliifanya na wala wasingelisita humo isipokuwa kidogo tu.



وَلَقَدْ كَانُوا عَاهَدُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ لَا يُوَلُّونَ الْأَدْبَارَ ۚ وَكَانَ عَهْدُ اللَّـهِ مَسْئُولًا ﴿١٥﴾
15. Na kwa yakini walikwishamuahidi Allaah kabla kwamba hawatogeuza migongo yao kukimbia. Na ahadi ya Allaah ni yenye kuulizwa daima.


قُل لَّن يَنفَعَكُمُ الْفِرَارُ إِن فَرَرْتُم مِّنَ الْمَوْتِ أَوِ الْقَتْلِ وَإِذًا لَّا تُمَتَّعُونَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٦﴾
16. Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Kukimbia hakutakufaeni ikiwa mmeyakimbia mauti, au kuuawa; kwani hamtostareheshwa isipokuwa kidogo tu.”



قُلْ مَن ذَا الَّذِي يَعْصِمُكُم مِّنَ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَ بِكُمْ سُوءًا أَوْ أَرَادَ بِكُمْ رَحْمَةً ۚ وَلَا يَجِدُونَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿١٧﴾
17. Sema: “Ni nani ambaye aweza kukulindeni na Allaah, kama Akikutakieni uovu au Akikutakieni rahmah?” Na wala hawatopata badala ya Allaah mlinzi na wala mwenye kunusuru.



قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الْمُعَوِّقِينَ مِنكُمْ وَالْقَائِلِينَ لِإِخْوَانِهِمْ هَلُمَّ إِلَيْنَا ۖ وَلَا يَأْتُونَ الْبَأْسَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٨﴾
18. Amekwishawajua Allaah miongoni mwenu wanaozuia (watu wasiende vitani) wanaowaambia ndugu zao: “Njooni kwetu!” Na hawaendi vitani isipokuwa kidogo tu.


أَشِحَّةً عَلَيْكُمْ ۖ فَإِذَا جَاءَ الْخَوْفُ رَأَيْتَهُمْ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ تَدُورُ أَعْيُنُهُمْ كَالَّذِي يُغْشَىٰ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ ۖ فَإِذَا ذَهَبَ الْخَوْفُ سَلَقُوكُم بِأَلْسِنَةٍ حِدَادٍ أَشِحَّةً عَلَى الْخَيْرِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَمْ يُؤْمِنُوا فَأَحْبَطَ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿١٩﴾
19. Wachoyo juu yenu; na inapokuja khofu utawaona wanakutazama macho yao yanazunguruka kama yule aliyefunikwa na mauti. Inapoondoka khofu wanakushutumuni kwa ndimi kali! Wachoyo wa kila kheri! Hao hawakuamini, basi Allaah Ameziporomosha ‘amali zao, na hayo kwa Allaah ni mepesi kabisa.



يَحْسَبُونَ الْأَحْزَابَ لَمْ يَذْهَبُوا ۖ وَإِن يَأْتِ الْأَحْزَابُ يَوَدُّوا لَوْ أَنَّهُم بَادُونَ فِي الْأَعْرَابِ يَسْأَلُونَ عَنْ أَنبَائِكُمْ ۖ وَلَوْ كَانُوا فِيكُم مَّا قَاتَلُوا إِلَّا قَلِيلًا ﴿٢٠﴾
20. Wanadhania kuwa makundi hayakuondoka bado. Na yanapokuja makundi, wanatamani lau kwamba wanaishi jangwani kwa mabedui; wanaulizia habari zenu. Na lau wangelikuwa wako pamoja nanyi, basi wasingelipigana isipokuwa kidogo tu.



لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا﴿٢١﴾
21. Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi.


وَلَمَّا رَأَى الْمُؤْمِنُونَ الْأَحْزَابَ قَالُوا هَـٰذَا مَا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَصَدَقَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ ۚ وَمَا زَادَهُمْ إِلَّا إِيمَانًا وَتَسْلِيمًا ﴿٢٢﴾
22. Basi Waumini walipoona makundi, walisema: “Haya ndio yale Aliyotuahidi Allaah na Rasuli Wake, na Amesema kweli Allaah na Rasuli Wake; na haikuwazidishia isipokuwa iymaan na kujisalimisha.


مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ ۖ فَمِنْهُم مَّن قَضَىٰ نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ ۖوَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلًا ﴿٢٣﴾
23. Miongoni mwa Waumini, wapo wanaume wamesadikisha yale waliyomuahidi Allaah; basi miongoni mwao aliyetimiza nadhiri yake; amekufa shahidi, na miongoni mwao wanaongojea na hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.


لِّيَجْزِيَ اللَّـهُ الصَّادِقِينَ بِصِدْقِهِمْ وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ إِن شَاءَ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٢٤﴾
24. Ili Allaah Awalipe wakweli kwa ukweli wao, na Awaadhibu wanafiki pindi Akitaka au Apokee tawbah yao. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuriaMwenye kurehemu. 


وَرَدَّ اللَّـهُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِغَيْظِهِمْ لَمْ يَنَالُوا خَيْرًا ۚ وَكَفَى اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ الْقِتَالَ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ قَوِيًّا عَزِيزًا ﴿٢٥﴾
25. Na Allaah Akawarudisha nyuma wale waliokufuru kwa ghaidhi zao hawakupata kheri yoyote. Na Allaah Amewatosheleza Waumini vitani. Na Allaah daima ni Mwenye nguvu zote, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika.


وَأَنزَلَ الَّذِينَ ظَاهَرُوهُم مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مِن صَيَاصِيهِمْ وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ فَرِيقًا تَقْتُلُونَ وَتَأْسِرُونَ فَرِيقًا ﴿٢٦﴾
26. Na Aliwateremsha wale waliowasaidia (maadui) miongoni mwa Ahlil-Kitaabi kutoka katika ngome zao; na Akavurumisha kizaazaa katika nyoyo zao; kundi mnaliua, na kundi jingine mnaliteka.


وَأَوْرَثَكُمْ أَرْضَهُمْ وَدِيَارَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ وَأَرْضًا لَّمْ تَطَئُوهَا ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرًا﴿٢٧﴾
27. Na Akakurithisheni ardhi yao, na majumba yao, na mali zao; na ardhi hamkuwahi kuzikanyaga; na Allaah daima ni Muweza juu ya kila kitu.



يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٢٨﴾
28. Ee Nabiy!  Waambie wake zako: “Ikiwa mnataka uhai wa dunia na mapambo yake; basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru, mwachano mzuri.


وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا﴿٢٩﴾
29. “Na ikiwa mnamtaka Allaah na Rasuli Wake na nyumba ya Aakhirah, basi hakika Allaah Amewaahidi wanawake watendao wema miongoni mwenu ujira adhimu.”


يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ مَن يَأْتِ مِنكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿٣٠﴾
30. Enyi wake wa Nabiy! Yeyote yule atakayeleta uchafu bayana miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu maradufu. Na hayo kwa Allaah ni mepesi.


وَمَن يَقْنُتْ مِنكُنَّ لِلَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتَعْمَلْ صَالِحًا نُّؤْتِهَا أَجْرَهَا مَرَّتَيْنِ وَأَعْتَدْنَا لَهَا رِزْقًا كَرِيمًا﴿٣١﴾
31. Na yeyote miongoni mwenu atakayemtii Allaah na Rasuli Wake, na akatenda mema; Tutampa ujira wake mara mbili, na Tumemuandalia riziki ya ukarimu.


يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ﴿٣٢﴾
32. Enyi wake wa Nabiy!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake; mkiwa na taqwa, basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika.


وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا ﴿٣٣﴾
33. Na bakieni majumbani mwenu, na wala msionyeshe mapambo na uzuri kwa ajinabi kujishaua kama zama za ujahili. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah na mtiini Allaah na Rasuli Wake. Hakika Allaah Anataka Akuondosheeni maovu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy) na Akutakaseni mtakaso barabara.


وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا ﴿٣٤﴾
34. Na kumbukeni yale yanayosomwa majumbani mwenu katika Ayaat za Allaah na Hikmah (Sunnah), hakika Allaah daima ni Mwenye kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.


إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾
35. Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, na wafungao Swawm wanaume na wanawake, wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu.


وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗوَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾
36. Na haiwi kwa Muumini mwanamme na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana.


وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِي أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّـهَ وَتُخْفِي فِي نَفْسِكَ مَا اللَّـهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَاهُ ۖ فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا لِكَيْ لَا يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِي أَزْوَاجِ أَدْعِيَائِهِمْ إِذَا قَضَوْا مِنْهُنَّ وَطَرًا ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ مَفْعُولًا ﴿٣٧﴾
37. Na pale ulipomwambia ambaye Allaah Amemneemesha nawe ukamneemesha: “Mshikilie mkeo, na mche Allaah!” Na ukaficha katika nafsi yako ambayo Allaah Ametaka kuyafichua, na unakhofu watu, na hali Allaah Ana haki zaidi umkhofu. Basi Zayd alipomaliza haja kwake Tukakuozesha ili isiwe dhambi juu ya Waumini kuhusu (kuoa) wake wa watoto wao wa kupanga wanapomaliza haja kwao. Na Amri ya Allaah daima ni yenye kutekelezwa.


مَّا كَانَ عَلَى النَّبِيِّ مِنْ حَرَجٍ فِيمَا فَرَضَ اللَّـهُ لَهُ ۖ سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا ﴿٣٨﴾
38. Hakuna dhambi yoyote juu ya Nabiy (kufanya) katika yale Aliyomfaridhishia Allaah, ni desturi ya Allaah kwa wale waliopita kabla. Na amri ya Allaah daima ni kudura iliyokwishakadiriwa vyema kabisa. 


الَّذِينَ يُبَلِّغُونَ رِسَالَاتِ اللَّـهِ وَيَخْشَوْنَهُ وَلَا يَخْشَوْنَ أَحَدًا إِلَّا اللَّـهَ ۗ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ حَسِيبًا ﴿٣٩﴾
39. Wale wanabalighisha ujumbe wa Allaah na wanamkhofu Yeye na wala hawamkhofu yeyote isipokuwa Allaah. Na Allaah Anatosheleza kuwa Mwenye kuhesabu.


مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٤٠﴾
40. Hakuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Rasuli wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu.



يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾
41. Enyi walioamini!  Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru.


وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾
42. Na Msabbihini asubuhi na jioni‏.



هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا﴿٤٣﴾
43. Yeye Ndiye Anakurehemuni, na Malaika Wake wanamuomba Akughufurieni na Akurehemuni ili Akutoeni kutoka katika viza kuingia katika Nuru. Naye daima ni Mwenye kurehemu Waumini.



تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾
44. Maamkizi yao Siku watakayokutana Naye; ni ‘Salaam’; na Amewaandalia ujira wa ukarimu.



يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿٤٥﴾
45. Ee Nabiy! Hakika Sisi Tumekutuma uwe shahidi, na mbashiriaji na mwonyaji.



وَدَاعِيًا إِلَى اللَّـهِ بِإِذْنِهِ وَسِرَاجًا مُّنِيرًا ﴿٤٦﴾
46. Na mlinganiaji kwa Allaah kwa idhini Yake; na siraji kali yenye nuru.



وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ بِأَنَّ لَهُم مِّنَ اللَّـهِ فَضْلًا كَبِيرًا ﴿٤٧﴾
47. Na wabashirie Waumini kwamba watapata kutoka kwa Allaah fadhila kubwa.



وَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَالْمُنَافِقِينَ وَدَعْ أَذَاهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿٤٨﴾
48. Na wala usiwatii makafiri na wanafiki, na achilia mbali maudhi yao, na tawakali kwa Allaah. Na Allaah Anatosheleza kuwa Mdhamini.



يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٤٩﴾
49. Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu. Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri.



يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَحْلَلْنَا لَكَ أَزْوَاجَكَ اللَّاتِي آتَيْتَ أُجُورَهُنَّ وَمَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ مِمَّا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَيْكَ وَبَنَاتِ عَمِّكَ وَبَنَاتِ عَمَّاتِكَ وَبَنَاتِ خَالِكَ وَبَنَاتِ خَالَاتِكَ اللَّاتِي هَاجَرْنَ مَعَكَ وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ إِنْ أَرَادَ النَّبِيُّ أَن يَسْتَنكِحَهَا خَالِصَةً لَّكَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۗ قَدْ عَلِمْنَا مَا فَرَضْنَا عَلَيْهِمْ فِي أَزْوَاجِهِمْ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ لِكَيْلَا يَكُونَ عَلَيْكَ حَرَجٌ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٠﴾
50. Ee Nabiy! Hakika Sisi Tumekuhalalishia wake zako ambao uliwapa mahari yao, na wale iliyomiliki mkono wako wa kuume katika wale (mateka) Aliokuruzuku Allaah, na mabinti wa ‘ammi zako, na mabinti wa mashangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa makhalati zenu ambao wamehajiri pamoja nawe, na mwanamke Muumini akijitunukia mwenyewe kwa Nabiy, ikiwa Nabiy anataka kumuoa. Ni makhsusi kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Tumekwishajua yale Tuliyowafaridhishia wao katika wake zao na wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume ili isijekuwa vigumu juu yako. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.


تُرْجِي مَن تَشَاءُ مِنْهُنَّ وَتُؤْوِي إِلَيْكَ مَن تَشَاءُ ۖ وَمَنِ ابْتَغَيْتَ مِمَّنْ عَزَلْتَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكَ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن تَقَرَّ أَعْيُنُهُنَّ وَلَا يَحْزَنَّ وَيَرْضَيْنَ بِمَا آتَيْتَهُنَّ كُلُّهُنَّ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا فِي قُلُوبِكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَلِيمًا ﴿٥١﴾
51. Umuakhirishie umtakaye miongoni mwao na umsogeze kwako umtakaye. Na ukimtaka katika uliyemtenga basi hakuna dhambi juu yako. Hivyo ni karibu zaidi kupelekea kuburudika macho yao, na wala wasihuzunike, na waridhike kwa yale uliyowapa kila mmoja wao. Na Allaah Anajua yale yaliyomo nyoyoni mwao. Na Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mvumilivu. 


لَّا يَحِلُّ لَكَ النِّسَاءُ مِن بَعْدُ وَلَا أَن تَبَدَّلَ بِهِنَّ مِنْ أَزْوَاجٍ وَلَوْ أَعْجَبَكَ حُسْنُهُنَّ إِلَّا مَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ رَّقِيبًا ﴿٥٢﴾
52. Si halali kwako wanawake wengine baada ya hao na wala kuwabadilisha kwa wake wengine japo kama uzuri wao umekupendeza isipokuwa wale iliyomiliki mkono wako wa kuume. Na Allaah daima ni Mwenye kuchunga kila kitu.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ ۖ وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ ۚ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا ﴿٥٣﴾
53. Enyi walioamini! Msiingie nyumba za Nabiy isipokuwa mkipewa idhini ya kwenda kula si kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni, na mkimaliza kula, tawanyikeni, na wala msikae kujiliwaza kwa mazungumzo. Hakika hiyo ilikuwa inamuudhi Nabiy, naye anakustahini, lakini Allaah Hasitahi (kubainisha) haki. Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Na haipasi kwenu kumuudhi Rasuli wa Allaah. Na wala kuwaoa wake zake baada yake abadani. Hakika jambo hilo mbele ya Allaah ni kubwa mno.


إِن تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٥٤﴾
54. Mkidhihirisha kitu chochote au mkikificha, basi hakika Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu.



لَّا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ ۗ وَاتَّقِينَ اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا ﴿٥٥﴾
55. Si dhambi juu yao wanawake kuonana na baba zao, na wala watoto wao wa kiume, na wala kaka zao, na wala watoto wa kiume wa kaka zao, na wala watoto wa kiume wa dada zao, na wala wanawake wenzao (wa Kiislamu), na wala iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah daima ni Mwenye kushuhudia kila kitu. 


إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
56. Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa.[1]



إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا ﴿٥٧﴾
57. Hakika wale wanaomuudhi Allaah na Rasuli Wake, Allaah Amewalaani duniani na Aakhirah, na Amewaandalia adhabu ya kudhalilisha.



وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٨﴾
58. Na wale wanaowaudhi Waumini wa kiume na Waumini wa kike bila ya kuwa wamechuma kosa, basi kwa yakini wamejibebea usingiziaji mkuu wa dhulma na dhambi bayana.



يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾
59. Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.



لَّئِن لَّمْ يَنتَهِ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْمُرْجِفُونَ فِي الْمَدِينَةِ لَنُغْرِيَنَّكَ بِهِمْ ثُمَّ لَا يُجَاوِرُونَكَ فِيهَا إِلَّا قَلِيلًا ﴿٦٠﴾
60. Ikiwa wanafiki, na wale ambao katika nyoyo zao mna maradhi, na waenezao fitnah katika Al-Madiynah hawatokoma, bila shaka Tutakusalitisha juu yao, kisha hawatokaa humo kuwa jirani zako isipokuwa kidogo tu.


مَّلْعُونِينَ ۖ أَيْنَمَا ثُقِفُوا أُخِذُوا وَقُتِّلُوا تَقْتِيلًا ﴿٦١﴾
61. Maluuni hao!  Popote wanapopatikana, wachukuliwe, na wauliwe mbali mauaji kamilifu.



سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾
62.  Ni desturi ya Allaah kwa wale waliopita kabla. Na wala hutopata mabadiliko katika desturi ya Allaah.


يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ ۚ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا﴿٦٣﴾
63. Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: “Ujuzi wake uko kwa Allaah.” Na nini kitakujulisha huenda Saa itakuwa karibu.

إِنَّ اللَّـهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا ﴿٦٤﴾
64. Hakika Allaah Amewalaani makafiri, na Amewaandalia moto uliowashwa vikali mno.


خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ لَّا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿٦٥﴾
65. Ni wenye kudumu humo abadi. Hawatopata mlinzi na wala mwenye kunusuru.


يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾
66. Siku zitakapopinduliwa nyuso zao motoni, watasema: “Laiti tungelimtii Allaah, na tungelimtii Rasuli.”


وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾
67. Na watasema: “Rabb wetu! Hakika sisi tumewatii mabwana zetu, na wakuu wetu, basi wametupoteza njia.”


رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾
68. “Rabb wetu! Wape adhabu maradufu, na walaani laana kubwa.”


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا ۚ وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا﴿٦٩﴾
69. Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliomuudhi Muwsaa, lakini Allaah Akamtoa tuhumanikutokana na yale waliyoyasema. Na alikuwa mbele ya Allaah mwenye kuheshimika.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾
70. Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli nyofu ya haki.


يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
71. Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu.



إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَن يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ ۖ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا ﴿٧٢﴾
72. Hakika Sisi Tulihudhurisha amana kwa mbingu na ardhi na majabali vikakataa kuibeba na vikaiogopa; lakini insani akaibeba. Hakika yeye amekuwa dhalimu mno, jahili mno.



لِّيُعَذِّبَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ وَيَتُوبَ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٣﴾
73. Ili Allaah Awaadhibu wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike, na washirikina wa kiume na washirikina wa kike; na Allaah Apokee tawbah ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike, na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.



 
[1] Faida:  Allaah (سبحانه وتعالى) kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  maana yake ni kumsifia kwa Malaika, kumteremshia rahmah na baraka, fadhila n.k. Ama Malaika Wake kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni kumuombea kwa Allaah (سبحانه وتعالى) du’aa Amghufurie na Amteremshie baraka. 

Tags

advertisement centil

This blog is created for your interest and in our interest as well as a website and social media sharing info Interest and Other Entertainment.