-->
logo

Kisa Cha Kuzaliwa Bibi Maryam Mama Yake Nabii 'Iysaa ('Alayhis-Salaam) Na Kulelewa Kwake

Hannah bint Faaquudh alikuwa mke wa  Bwana 'Imraan. Imesemekena kwamba alikuwa hakujaaliwa kupata watoto na kwamba siku moja aliona ndege akimlisha  kinda chake. Alipoona hivyo akatamani sana kupata mtoto akaomba Du'aa kwa Allaah سبحانه وتعالى Amjaalie kizazi. Allaahسبحانه وتعالى Akamtakabalia Du'aa yake akashika mimba. Akaweka nadhiri kumfanya mwanawe awe mwenye kumakinika katika ibada na kuihudumia Baytul-Maqdis (Msikiti wa Aqswaa). Hivyo alipotambua kuwa amekwishabeba mimba akaweka hiyo nadhiri. 
((إِذْ قَالَتِ امْرَأَةُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ))
((Aliposema mke wa 'Imraan: Mola wangu! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua)) [Al-'Imraan:35]
Maana kwamba Wewe Unasikia Du'aa yangu na Unatambua niya yangu. Hakujua kama atajaaliwa mtoto wa kiume au wa kike. Alipojifungua mtoto wa kike aliona kwamba mwanamke sio kama mwanamume kwa kukusudia katika kujifunga na ibada msikitini.  
((فَلَمَّا وَضَعَتْهَا قَالَتْ رَبِّ إِنِّي وَضَعْتُهَا أُنثَى وَاللّهُ أَعْلَمُ بِمَا وَضَعَتْ وَلَيْسَ الذَّكَرُ كَالأُنثَى وَإِنِّي سَمَّيْتُهَا مَرْيَمَ وِإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ))
((Basi alipomzaa alisema: Mola wangu! Nimemzaa mwanamke - na Allaah Anajua sana aliyemzaa - Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na mimi nimemwita Maryam. Nami namkinga Kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na shaytwaan aliyelaaniwa)) [Al-'Imraan:36]
Maryam maana yake ni 'Mtumishi wa Allaah'.
Aayah hiyo inathibitisha kuruhusiwa kumpa jina mtoto siku ile ile anayozaliwa (kama ambavyo imethibiti kumpa jina mtoto katika siku ya saba wakati wa kumfanyia 'Aqiyqah), na vile vile ni dhahiri katika Aayah hii kwamba hii ilikuwa pia ni sheria ya watu waliokuwa kabla yetu.  Na pia iko katika Sunnah ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  aliposema:
 ((وُلِدَ لِي اللَّيْلَةَ وَلَد سَمَّيْتُهُ بِاسْمِ أبِي إبْرَاهِيمَ))
((Usiku huu mtoto (wa kiume) amezaliwa kwangu na nimemwita jina la baba yangu Ibraahiym))[Al-Bukhaariy na Muslim]
Kama Aayah ilivyomalizikia kwamba Bibi Hannah alimuomba  Allaah سبحانه وتعالى Amkinge na shaytwaan. Allaah سبحانه وتعالى Akamtakabalia Du'aa yake na dalili ni Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه
 ((مَا مِن مَوْلُودٍ يُولَدُ إلا مَسَّه الشَّيْطَانُ حِينَ يُولَدُ، فَيَسْتَهِلّ صَارخًا مِنْ مَسِّهِ إيَّاهُ، إلا مَرْيَم َوابْنَهَا)) ثم يقول أبو هريرة: اقرأوا إن شئتم(( وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيم))ِ))
((Hakuna kizazi chochote kinachozaliwa ila shaytwaan anakigusa kinapozaliwa, na mtoto huanza kulia kwa sababu ya kuguswa huko, isipokuwa Maryam na mtoto wake [yaani 'Iysa عليه السلام]
Abu Hurayrah kisha akasema someni mkipenda: ((Nami namkinga Kwako, yeye na uzao wake, Uwalinde na shaytwaan aliyelaaniwa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Akapelekwa Maryam tokea utoto wake msikitini na akakulia huko na akamtoa kama ni zawadi ya Baytul-Maqdis.
Waliokuwa na jukumu la kuihudumia Baytul-Maqdis waligombania kumlea Maryam baada ya kufariki baba yake. Walisema kwamba kwa-vile ni mtoto wa Bwana 'Imraan ambaye alikuwa ni Imaam wao basi ni jukumu lao kumlea. Zakariyah عليه السلام naye akadai kumlea Maryam akasema: "Nipeni mimi kwani ndugu wa mama yake ni mke wangu". Wakasema: "Nyoyo zetu hazitopenda umlee wewe kwa sababu ni mtoto wa Imaam wetu". Ikabidi wafanye kura ya kutupa kalamu zao walizokuwa wakiandikia Taurati katika mto wa Jordan. Yule ambaye kalamu yake itaelea katika mto ndiye atakayemlea Maryam.  Walipozitupa kalamu zao, zote zilizama isipokuwa ya Zakariyyah  عليه السلام ambaye pia naye alikuwa ni bwana wao, Mwanachuoni wao na pia ni Mtume wao. 
Allaah سبحانه وتعالى Anampa kisa hiki Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika wahyi (ufunuo) kisha  Anawatanabahisha makafiri  kwamba hizi ni habari za ghaibu ambazo hakuzijua Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kabla, na kwa maana kwamba haya maelezo ya Qur-aan si maneno ya Mtume kama wanavyodai makafiri:
((ذَلِكَ مِنْ أَنبَاء الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيكَ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يُلْقُون أَقْلاَمَهُمْ أَيُّهُمْ يَكْفُلُ مَرْيَمَ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يَخْتَصِمُونَ))
((Hizi ni khabari za ghaibu tunazokufunulia; nawe hukuwa nao walipokuwa wakitupa kalamu zao nani wao atamlea Maryam, na hukuwa nao walipokuwa wakishindana)) [Al-'Imraan: 44]
Tukirudia kisa alipozaliwa Maryam, Allaah سبحانه وتعالى Alikubali nadhiri ya mama yake Akamjaaliya kuwa na tabia njema na kupata elimu ya dini yake kutoka kwa Nabii Zakariyyah عليه السلام hata akawa mcha Mungu sana na akapata sifa ya 'utiifu' kama alivyotajwa katika Aayah hizo za juu. Kutwa kucha alikuwa akifanya ibada. Ikawa kila mara Zakariyyah عليه السلام anapoingia katika mihraab (sehemu yake aliyokuwa akiswalia) anamkuta ana matunda ya ajabu. Kwa maana kwamba msimu wa baridi anamkuta ana matunda ya msimu wa joto na msimu wa joto anamkuta ana matunda ya msimu wa baridi ndipo alipomuuliza kama yanavyokuja maelezo katika Aayah ifuatayo:
((فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ وَجَدَ عِندَهَا رِزْقاً قَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّى لَكِ هَذَا قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللّهِ إنَّ اللّهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاء بِغَيْرِ حِسَاب))
((Tena Mola wake Akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariyyah awe mlezi wake. Kila mara Zakariyyah alipoingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ee Maryam! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Allaah; na Allaah Humruzuku Amtakaye bila ya hisabu)) [Al-'Imraan: 37]
[Kisa kama kilivyonukuliwa katika tafsiyr ya Ibn Kathiyr


لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ ِلأُوْلِي الأَلْبَابِ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَى وَلَكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Kwa hakika katika visa vyao yamo mazingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.  [Yuwsuf: 111]

Tags

advertisement centil

This blog is created for your interest and in our interest as well as a website and social media sharing info Interest and Other Entertainment.