Kauli zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
أَمْ حَسِبْتَ أَنَّ أَصْحَابَ الْكَهْفِ وَالرَّقِيمِ كَانُوا مِنْ آيَاتِنَا عَجَبًا ﴿٩﴾إِذْ أَوَى الْفِتْيَةُ إِلَى الْكَهْفِ فَقَالُوا رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا ﴿١٠﴾فَضَرَبْنَا عَلَىٰ آذَانِهِمْ فِي الْكَهْفِ سِنِينَ عَدَدًا ﴿١١﴾ثُمَّ بَعَثْنَاهُمْ لِنَعْلَمَ أَيُّ الْحِزْبَيْنِ أَحْصَىٰ لِمَا لَبِثُوا أَمَدًا ﴿١٢﴾نَّحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ نَبَأَهُم بِالْحَقِّ ۚ إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى ﴿١٣﴾وَرَبَطْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ إِذْ قَامُوا فَقَالُوا رَبُّنَا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَن نَّدْعُوَ مِن دُونِهِ إِلَـٰهًا ۖ لَّقَدْ قُلْنَا إِذًا شَطَطًا ﴿١٤﴾ هَـٰؤُلَاءِ قَوْمُنَا اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً ۖ لَّوْلَا يَأْتُونَ عَلَيْهِم بِسُلْطَانٍ بَيِّنٍ ۖ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ﴿١٥﴾ وَإِذِ اعْتَزَلْتُمُوهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّـهَ فَأْوُوا إِلَى الْكَهْفِ يَنشُرْ لَكُمْ رَبُّكُم مِّن رَّحْمَتِهِ وَيُهَيِّئْ لَكُم مِّنْ أَمْرِكُم مِّرْفَقًا ﴿١٦﴾
9. Je, unadhani kwamba watu wa pangoni na maandiko walikuwa ni ajabu miongoni mwa Aayaat (miujiza, ishara) Zetu? 10. Pale vijana walipokimbilia katika pango wakasema: Rabb wetu! Tupe kutoka Kwako rahmah, na Tutengenezee katika jambo letu mwongozo wa sawa. 11. Tukawaziba masikio yao pangoni (kuwalaza) kwa idadi ya miaka mingi. 12. Kisha Tukawainua ili Tujue nani kati ya makundi mawili lilohesabu madhubuti zaidi kuhusu muda wao waliobakia. 13. Sisi Tunakusimulia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari zao kwa haki. Hakika wao ni vijana waliomwamini Rabb wao; na Tukawazidishia Uongofu. 14. Na Tukazitia nguvu nyoyo zao waliposimama wakasema: Rabb wetu, ni Rabb wa mbingu na ardhi. Hatutomuomba asiyekuwa Yeye kuwa mwabudiwa, (laa sivyo) kwa yakini hapo tutakuwa tumesema kauli ya kufuru na kuvuka mpaka. 15. Hawa watu wetu wamejichukulia waabudiwa wengine badala Yake. Kwa nini basi hawawatolei ushahidi wa bayana? Basi nani dhalimu zaidi kuliko anayemtungia Allaah uongo? 16. Na mkijitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Allaah; basi kimbieni pangoni; Rabb wenu Atakufungulieni rahmah Zake, na Atakutengenezeeni wepesi katika mambo yenu. [Al-Kahf: 9-16]
Maelezo Kwa Ufupi Kuhusu Kisa Hiki:
Kisa hiki ni kuhusu vijana walioamini Tawhiyd (kumpwekesha Allaah) wakajitenga na ‘ibaadah ya masanamu, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akazidi kuwaongoa. Vijana hao walikuwa wakiishi katika mji ambao mfalme wao alikuwa akiabudu masanamu. Alivyojua huyo mfalme kwamba hawa vijana wamekanusha ‘ibaadah yao ya masanamu, na baada ya kujua sababu zao, akataka kuwadhulumu kwa kuwatesa na kuwaua.
Wakakimbilia katika pango ambapo humo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwateremshia Rahma Yake kwa kuwahifadhi na kuwaficha humo wasijulikane.
Akawapa usingizi wa kulala miaka zaidi ya mia tatu, ili watakapoamka hatokuweko tena huyo mfalme wala kizazi chochote kilichowahi kuwepo wakati huo walipokimbia.
Maelezo zaidi ya kisa hiki ni kama kilivyotajwa katika Aayah zifuatazo:
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaanza kutusimulia kisa hiki cha Asw-haabul-Kahf kwa kuwauliza Makafiri wa Quraysh:
أَمْ حَسِبْتَ أَنَّ أَصْحَابَ الْكَهْفِ وَالرَّقِيمِ كَانُوا مِنْ آيَاتِنَا عَجَبًا ﴿٩﴾
9. Je, unadhani kwamba watu wa pangoni na maandiko walikuwa ni ajabu miongoni mwa Aayaat (miujiza, ishara) Zetu?
Anatuelezea kwamba kisa chao sio jambo la kustaajabisha kulinganisha na Qudra Yake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Hikma Yake. Hivyo kwa sababu Yeye Ndiye Muumba wa kila kitu; Ameumba mbingu na ardhi, Anajaalia kubadilika mchana na usiku, kutiishwa kwa jua na mwezi, Anaweza kumfisha aliye hai na Akamfufua aliyekufa. Vilioko mbinguni vyote, na vinginevyo Alivyoviumba vinadhihirisha Utukufu na Nguvu Zake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kwamba Yeye Anaweza kufanya lolote Alitakalo. Kwa hiyo, miujiza ya kisa cha Asw-haabul-Kahf si lolote Kwake Ameshafanya miujiza zaidi ya haya.
Ibn Jurayr alimsikia Mujaahid akisema kuhusu Aayah hiyo kwamba ina maana: "Miongoni mwa Aayaat (Ishara) Zetu kuna maajabu zaidi ya haya." [Atw-Twabariy 17:601].
Al-'Awf ameeleza maelezo kutoka kwa Ibn ‘Abbaas ambaye alisema: kuhusu Aayah hiyo kwamba ina maana: "Yale niliyokupa ya elimu, Qur-aan na Sunnah ni bora zaidi kuliko kisa cha Asw-haabul-Kahf na Ar-Raqiym."
Maana ya Al-Kahf na Ar-Raqiym:
Al-Kahf ni pango katika jabali ambalo vijana hao walikimbilia kujificha humo. Na kuhusu neno la 'Ar-Raqiym' kuna kauli mbali mbali za Salaf kama ifuatavyo:
Al-‘Awfi amemsikia Ibn 'Abbaas kwamba: “Ni bonde karibu na Aylah.” Hii imesimuliwa pia kwengine na 'Atwiyyah, Al-'Awfi pamoja na Qataadah.
Adh-Dhwahhaak kasema: “Al-Kahf ni pango katika bonde na Ar-Raqiym ni jina la bonde.”
Mujaahid kasema: “Ar-Raqiym inakusudiwa majengo yao.”
Wengine wamesema kuwa: “Ni bonde ambalo lilikuwepo hilo pango lao.”
Ka'ab alikuwa akisema kwamba: “Ni mji.”
Ibn Jariyr kaeleza kwamba Ibn 'Abbaas kasema: “Ar-Raqiym ni jabali lilokuwemo hilo pango.”
Sa'iyd bin Jubayr kasema: “Ar-Raqiym ni ubamba wa jiwe wenye maandiko walioandikia kisa cha Asw-haabul-Kahf kisha wakaliweka katika kiingilio cha mlango wa pango.” [Atw-Twabariy 17: 601 – 603].
Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
إِذْ أَوَى الْفِتْيَةُ إِلَى الْكَهْفِ فَقَالُوا رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا ﴿١٠﴾
10. Pale vijana walipokimbilia katika pango wakasema: Rabb wetu! Tupe kutoka Kwako rahmah, na Tutengenezee katika jambo letu mwongozo wa sawa.
Hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuelezea kuhusu hao vijana wa kiume waliowakimbia watu wao kwa sababu ya dini yao potofu kwamba wamekimbia kwa kuogopa kuuliwa, kwa hiyo wakakimbilia pangoni katika mlima na kujificha humo. Walipoingia pangoni wakamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Awateremshie Rahmah na huruma kwao wakasema:
رَبَّنَا آتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً … ﴿١٠﴾
Rabb wetu! Tupe kutoka Kwako rahmah
Kwa maana: Tupe Rahmah na Utufiche na watu wetu.
وَهَيِّئْ لَنَا مِنْ أَمْرِنَا رَشَدًا ﴿١٠﴾
Na Tutengenezee katika jambo letu mwongozo wa sawa.
Maana: Yaelekeze mambo vizuri kwa kutujaalia mwisho mwema. Hivyo ni kama maana inayotokana na Hadiyth ifuatayo:
وَمَاَ قَضَيْتَ لَنَا مِنْ قَضَاءٍ فَاجْعَلْ عَاقِبَتَهُ رَشَداً
Na lolote Utakalotuamulia, basi Lijaalie liwe na mwisho mwema.
Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
فَضَرَبْنَا عَلَىٰ آذَانِهِمْ فِي الْكَهْفِ سِنِينَ عَدَدًا ﴿١١﴾
11. Tukawaziba masikio yao pangoni (kuwalaza) kwa idadi ya miaka mingi.
Kwa maana: Tukawafanya walale walipoingia pangoni, na wakalala miaka mingi.
Kawaida ya mtu anapolala hufunga macho yake na si masikio. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kuwa Aliwazibua masikio yao. Hii ni kutokana na Hikmah kubwa Aliyoitumia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutaja kuwazibua masikio yao. Hivyo kuna mafunzo ya kuzingatia kuhusu umuhimu wa ‘sikio’, miongoni mwa viungo vya mwili wa bin-Aadam. (Mazingatio na faida hizo ziko mwisho wa Makala hii):
Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuhusu Asw-haabil-Kahf zinaendelea:
ثُمَّ بَعَثْنَاهُمْ لِنَعْلَمَ أَيُّ الْحِزْبَيْنِ أَحْصَىٰ لِمَا لَبِثُوا أَمَدًا ﴿١٢﴾
12. Kisha Tukawainua ili Tujue nani kati ya makundi mawili lilohesabu madhubuti zaidi kuhusu muda wao waliobakia.
Maana ya:
لِنَعْلَمَ أَيُّ الْحِزْبَيْنِ ﴿١٢﴾..
ili Tujue nani kati ya makundi mawili
Makundi yaliyobishana kuhusu Asw-haabul-Kahf.
أَحْصَىٰ لِمَا لَبِثُوا أَمَدًا ﴿١٢﴾
12. Lilohesabu madhubuti zaidi kuhusu muda wao waliobakia.
Inakusudiwa mabishano kuhusu muda waliokaa katika pango.
نَّحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ نَبَأَهُم بِالْحَقِّ ۚ إِنَّهُمْ فِتْيَةٌ آمَنُوا بِرَبِّهِمْ وَزِدْنَاهُمْ هُدًى ﴿١٣﴾
13. Sisi Tunakusimulia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari zao kwa haki. Hakika wao ni vijana waliomwamini Rabb wao; na Tukawazidishia Uongofu. [Al-Kahf: 13]
Hapa ndipo kinapoanza kusimuliwa kwa urefu kisa chao vijana hao. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamwambia Rasul Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba, hiki ni kisa cha kweli kisichokuwa na shaka. Walikuwa ni vijana walioamini Tawhiyd (kumpwekesha Allaah) na wakajiweka mbali na shirki iliyotendwa na watu wa mji wao. Aghlabu vijana huwa wepesi kuitikia na kufuata haki kuliko wazee. Hivi ni kama ilivyokuwa hali ya watu wa kale kama Aayah zifuatazo zinavyothibitisha:
فَمَا آمَنَ لِمُوسَىٰ إِلَّا ذُرِّيَّةٌ مِّن قَوْمِهِ عَلَىٰ خَوْفٍ مِّن فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِمْ أَن يَفْتِنَهُمْ ۚ ﴿٨٣﴾
83. Basi hawakumwamini Muwsaa isipokuwa dhuriya katika kaumu yake kwa sababu ya kumkhofu Fir’awn na wakuu wao wasiwatese. [Yuwnus: 83]
Ilikuwa ni aghlabu kuwa vijana ndio waliokuwa wakipendelea kuitikia wito wa Rusuli wa Allaah. Ama wazee kwa kuwa wamebobea katika itikadi zao za kale, ikawa ni shida na muhali kwao kuacha waliyokuwa wakiyafuata ya mababu zao.
Vile vile, ukirejea Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) utaona kuwa wengi wa walioitikia Uislaam walikuwa ni vijana. Ama wazee wa ki-Quraysh walipendelea kubakia katika dini yao ila wachache mno.
Hali hii inadhihirika katika zama zetu kwamba si wepesi wazee kufuata haki pale wanapokatazwa kufuata yasiyomo katika Dini, kwa sababu wanaona vigumu kuacha mafunzo na mila walizokulia nazo za mababu na mashekhe wao.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaendelea kutaja kwamba Aliwaongezea uongofu kwa vile wenyewe walipenda uongofu.
وَزِدْنَاهُمْ هُدًى ﴿١٣﴾
13. na Tukawazidishia Uongofu.
Pia, Ametaja hivyo katika kauli Zake nyenginezo zifuatazo:
وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ﴿١٧﴾
17. Na wale walioongoka, Anawazidishia Uongofu na Huwajazi taqwa yao. [Muhammad: 17].
Na pia,
هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ ۗ وَلِلَّـهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا﴿٤﴾
4. Yeye Ndiye Aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili Awazidishie iymaan pamoja na iymaan zao. [Al-Fat-h: 4]
Aayah kuhusu Asw-haabul-Kahf zinaendelea:
وَرَبَطْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ إِذْ قَامُوا فَقَالُوا رَبُّنَا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَن نَّدْعُوَ مِن دُونِهِ إِلَـٰهًا ۖ لَّقَدْ قُلْنَا إِذًا شَطَطًا ﴿١٤﴾
14. Na Tukazitia nguvu nyoyo zao waliposimama wakasema: Rabb wetu, ni Rabb wa mbingu na ardhi. Hatutomuomba asiyekuwa Yeye kuwa mwabudiwa, (laa sivyo) kwa yakini hapo tutakuwa tumesema kauli ya kufuru na kuvuka mpaka.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwapa nguvu na iymaan zaidi wawe dhidi ya watu wa mji wao, waachilie mbali starehe ya maisha waliyokuwa nayo.
Baadhi ya Wafasiri wa Qur-aan wamesema kuwa walikuwa wana wa wafalme ambao ni wakuu wa Byantium. Siku moja walikwenda katika sikukuu ya watu wao waliokuwa wakikusanyika mara moja kwa mwaka nje ya mji, kisha wakiabudu masanamu na kuwachinjia kafara. Mfalme wao alikuwa dhalimu, mjeuri, akiitwa Decianus na alikuwa akiwalazimisha watu waende kwenye sherehe hizo.
Vijana hao walipokwenda na wazee wao katika sherehe hizo na walipoona ‘ibaadah zinazofanywa kwa ajili ya masanamu; kusujudiwa na kuchinjiwa kafara, walitambua kuwa ni jambo lisilopasa kwani ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Muumba wa kila kitu.
Akawa anaondoka mmoja baada ya mmoja kujitenga mbali na watu wao. Wa kwanza aliyejitenga alikwenda kukaa chini ya mti wenye kivuli. Kisha akaja mwengine kukaa naye, kisha akaja mwengine tena, kisha wakafuatia wengine wanne. Wote walikuwa hawajuani lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwaunganisha pamoja kutokana na iymaan zao. Hiyo ni Rahmah Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama ilivyothibiti katika Hadiyth iliyopokelewa toka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) ambaye amesema:
سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ : ((الأَرْوَاحُ جُنُودٌ مُجَنَّدَةٌ فَمَا تَعَارَفَ مِنْهَا ائْتَلَفَ وَمَا تَنَاكَرَ مِنْهَا اخْتَلَفَ (( صحيح البخاري : كتاب أحاديث الأنبياء : باب الأرواح جنود مجندة .
Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Roho ni kama askari waliokusanyana, zile zinazotambuana zinakutana pamoja, na zile zisizotambuana zinatengana)) [Al-Bukhaariy]
Kila mmoja wao hao vijana, alijaribu kuficha iymaan yake kwa mwenziwe kwa khofu ya kujulikana na mfalme na watu wao. Mmoja wao akaanza kusema "Enyi watu, bila ya shaka mnajua kuwa ni sababu fulani iliyokufanyeni mujitenge na watu wetu, basi hebu kila mmoja aelezee sababu yake." Mmoja wao akasema: "Mimi kwa hakika nilivyoona wanayoyatenda watu wangu, nimetambua ni makosa, na kwamba apasae kutendewa hayo ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee bila ya kumshirikisha na chochote. Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake.”
Wa pili akasema: "Mimi hali kadhalika ni sababu hiyo hiyo." Kisha wengine wote wakakiri kuwa ni sababu hiyo hiyo iliyowafanya kutengana na watu kutokana na kuchukiwa kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa ‘ibaadah zao za masanamu.
Vijana hao, wakatafuta sehemu maalumu ya kufanya ‘ibaadah yao kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Lakini watu wao wakaja kujua, wakamwambia mfalme ambaye aliamrisha waletwe mbele yake na kuwauliza kuhusu itikadi yao. Vijana hao hawakuogopa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwatia nguvu na kuwazidishia iymaan waseme ukweli wao kama Anavyosema:
وَرَبَطْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ إِذْ قَامُوا فَقَالُوا رَبُّنَا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَن نَّدْعُوَ مِن دُونِهِ إِلَـٰهًا ۖ لَّقَدْ قُلْنَا إِذًا شَطَطًا ﴿١٤﴾
14. Na Tukazitia nguvu nyoyo zao waliposimama wakasema: Rabb wetu, ni Rabb wa mbingu na ardhi. Hatutomuomba asiyekuwa Yeye kuwa mwabudiwa, (laa sivyo) kwa yakini hapo tutakuwa tumesema kauli ya kufuru na kuvuka mpaka.
Maana ya:
لَّقَدْ قُلْنَا إِذًا شَطَطًا ﴿١٤﴾
Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.
Yaani: Tutasema jambo sio la ukweli na tutakuwa tunasema uongo.
Wakaendelea kusema vijana:
هَـٰؤُلَاءِ قَوْمُنَا اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً ۖ لَّوْلَا يَأْتُونَ عَلَيْهِم بِسُلْطَانٍ بَيِّنٍ ۖ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ﴿١٥﴾
15. Hawa watu wetu wamejichukulia waabudiwa wengine badala Yake. Kwa nini basi hawawatolei ushahidi wa bayana? Basi nani dhalimu zaidi kuliko anayemtungia Allaah uongo? [Al-Kahf:14]
Yaani: Kwa nini hawatoi uthibitisho ulio dhahiri wa halisi kwa tabia yao hiyo?
فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ﴿١٥﴾
Basi nani dhalimu zaidi kuliko anayemtungia Allaah uongo?
Imesemekana kwamba walivyomtaka mfalme amuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), alikataa, akawaonya na kuwatisha. Aliamrisha wavuliwe nguo na wavalishwe mapambo ya watu wao. Kisha akawapa muda wafikirie hali zao huku akitumainia kuwa watarudi katika dini yao.
Wakakimbia kuepukana kuuliwa. Hali kama hii inakubalika katika Shariy’ah ya Kiislaam. Anaruhusiwa mtu pale anapokhofia kuwa fitnah itampelekea kupoteza Dini Yake. Imepokelewa toka kwa Sa’iyd al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
يُوشِكُ أَنْ يَكُونَ خَيْرَ مَالِ الْمُسْلِمِ غَنَمٌ يَتْبَعُ بِهَا شَعَفَ الْجِبَالِ ، وَمَوَاقِعَ الْقَطْرِ يَفِرُّ بِدِينِهِ مِنَ الْفِتَنِ
“Inakaribia kuwa mali bora kabisa ya Muislaam itakuwa ni kondoo hufuatwa juu ya milima na sehemu zinazomwagika maji (anakimbia) asiuliwe kwa sababu ya Dini yake.” [Al-Bukhaariy].
Kwa hali kama hiyo ya kukhofia Dini yake mtu, inaruhusiwa kujitenga mbali na watu. Vinginevyo, haifai kwa sababu Muislamu atapoteza faida za Swalaah za Jama’aah.
Vijana hawa waliazimia kuwakimbia watu wao. Ilikuwa ni Qadhwaa na Qadar (Yaliyopangwa na Makadirio) ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na ndio maana ikasemwa:
وَإِذِ اعْتَزَلْتُمُوهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّـهَ فَأْوُوا إِلَى الْكَهْفِ يَنشُرْ لَكُمْ رَبُّكُم مِّن رَّحْمَتِهِ وَيُهَيِّئْ لَكُم مِّنْ أَمْرِكُم مِّرْفَقًا ﴿١٦﴾
16. Na mkijitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Allaah; basi kimbieni pangoni; Rabb wenu Atakufungulieni rahmah Zake, na Atakutengenezeeni wepesi katika mambo yenu. [Al-Kahf:16]
Maana: Mkijitenga nao kwa sababu ya kuikanusha dini yao ya kuabudu ghairi ya Allaah, basi jitengeni nao kwa kuwa mbali nao kabisa, hivyo kimbilieni kwenye pango kisha hapo:
يَنشُرْ لَكُمْ رَبُّكُم مِّن رَّحْمَتِهِ … ﴿١٦﴾
16. Rabb wenu Atakufungulieni rahmah Zake.
Yaani: Atakuteremshieni Rahmah Yake. Nayo ni kuwaficha ili msijulikane na watu wenu.
وَيُهَيِّئْ لَكُم مِّنْ أَمْرِكُم مِّرْفَقًا ﴿١٦﴾
Na Akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu.
Yaani: Atakupeni yale mnayoyahitaji.
Wakakimbia pangoni kujificha. Kisha watu wao wakaanza kuhisi kupotea kwao. Mfalme akatuma watu kuwatafuta, lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Aliwaficha wasionekane. Hawakuweza kupata alama yoyote au kusikia habari yoyote yao baada ya hapo.
Hivyo ni kama pale Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) walipojificha katika pango la at-Thawr walipokuwa wanahajiri kuelekea Madiynah, wakati makafiri wakiwatafuta. Hawakuweza kuwaona japokuwa walipita chini ya pango hilo. Abu Bakr aliingiwa na khofu ya kujulikana akasema: "Ee Rasuli wa Allaah, mmoja wao akitazama chini atatuona". Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
يَا أَبا بَكْرٍ مَا ظَنُّكَ بِإثْنَيْنِ اللَّهُ ثاَلِثُهُماَ؟
Ee Abu Bakr, unafikiriaje wawili ambao wanaye Allaah kuwa ni watatu wao?
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametaja kunusurika kwao:
إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٤٠﴾
40. Msipomnusuru (Rasuli), basi Allaah Amekwishamnusuru, pale walipomtoa (Makkah) wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili; walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi. Basi Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona, na Akajaalia neno la waliokufuru kuwa chini. Na Neno la Allaah kuwa ndilo lililo juu. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 40]
Faida Na Mazingatio: Muujiza Wa Qur-aan Inapotajwa Kuhusu "Sikio":
Ili kufahamika vizuri sababu ya Aswaabul-Kahf kulazwa miaka mingi, maswali yafuatayo yanatoa mwanga:
1-Kiungo gani kilicho muhimu zaidi kati ya macho na sikio? Kwa maana ikiwa kuna chaguo la kukosa mojawapo, kipi kitakuwa ni shida mno kwa mtu kukisoa? Bila ya shaka ni macho. Kwa sababu kuwa kiziwi ni sahali kuliko kuwa kipofu. Lakini tunaona katika Qur-aan kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatanguliza kutaja (kusikia) kabla ya (kuona au macho) katika Aayah zinazotaja viungo viwili hivyo.
2- Kwa nini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anataja
السمع
Kusikia
Kwa umoja (singular) na
أبصار
kuona au macho
Kwa wingi kama inavyotajwa katika Aayah zifautazo:
وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَـٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّـهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ﴿٢٢﴾
22. Na hamkuwa mkijisitiri hata yasishuhudie masikio yenu, na wala macho yenu, na wala ngozi zenu; lakini mlidhania kwamba Allaah Hajui mengi katika yale mnayoyatenda. [Fusswilaat: 22]
Na pia Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَلَقَدْ مَكَّنَّاهُمْ فِيمَا إِن مَّكَّنَّاكُمْ فِيهِ وَجَعَلْنَا لَهُمْ سَمْعًا وَأَبْصَارًا وَأَفْئِدَةً فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُمْ سَمْعُهُمْ وَلَا أَبْصَارُهُمْ وَلَا أَفْئِدَتُهُم مِّن شَيْءٍ إِذْ كَانُوا يَجْحَدُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴿٢٦﴾
26. Na kwa yakini Tuliwamakinisha katika ambayo Hatukumakinisheni humo (nyinyi Maquraysh); na Tukawajaalia masikio na macho na nyoyo za kutafakari; lakini hayakuwafaa chochote masikio yao na wala macho yao na wala nyoyo zao za kutafakari walipokuwa wakikanusha kwa ujeuri Aayaat (hoja, ishara) za Allaah na yakawazunguka ambayo walikuwa wakiyafanyia istihzai. [Al-Ahqaaf: 26].
Na pia,
قُلْ هُوَ الَّذِي أَنشَأَكُمْ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۖ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ﴿٢٣﴾
23. Sema: Yeye Ndiye Yule Aliyekuanzisheni na Akakujaalieni kusikia na kuona na nyoyo za kutafakari. Ni kidogo sana mnayoshukuru. [Al-Mulk 23].
Majibu:
i) Sikio ni kiungo cha mwanzo kabisa kufanya kazi katika mwili wa mwana-Aadam anapozaliwa. Tunajua kuwa mtoto mchanga huchelewa kidogo kuona, lakini hachelewi kusikia kwani anaweza kuamka inapomfikia sauti kubwa.
ii) Pia, sikio ni kiungo cha mwanzo kitakachofanya kazi Siku ya Qiyaamah pale Malaaika Israafiyl atakapopiga as-swuwr (baragumu), likasikika kwa viumbe wote na ndipo watakapofufuka watu kutoka makaburini mwao. Wengine watazimia kutokana na ukali wa sauti hiyo ya baragumu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَيَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ ﴿٨٧﴾
87. Na Siku itakayopulizwa baragumu, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini isipokuwa Amtakaye Allaah. Na wote watamfikia wakiwa duni wamedhalilika. [An-Naml: 87].
Anasema pia:
يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ ۚ وَنَحْشُرُ الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ زُرْقًا ﴿١٠٢﴾
102. Siku itakayopulizwa katika baragumu. Na Tutawakusanya wakhalifu Siku hiyo hali macho yao yatakuwa rangi ya buluu (kwa kiwewe). [Twaahaa: 102].
Na pia Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَتَأْتُونَ أَفْوَاجًا ﴿١٨﴾
18. Siku itakayopulizwa katika baragumu, mtakuja makundi makundi. [An-Nabaa: 18].
iii) Sikio ni kiungo cha mwisho kabisa kusita kufanya kazi mtu anapofariki, kwa sababu kuna dalili kwamba mtu anapofariki huwa anasikia kila kitu hadi anapotiwa kaburini kwa muda fulani.
iv) Ili mtu aweze kuona, anahitaji mwanga kwani kizani hawezi kuona. Lakini masikio yanafanya kazi wakati wowote au mahali popote. Mfano anapolala mtu hufumba macho. Lakini masikio yanafanya kazi yake ya kusikia wakati wowote. Ndio maana mwizi anapoingai katika nyumba kutaka kuiba hunyata polepole ili asisikie mtu. Na Allaah Anathibitisha kwa kusema:
وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ ۖ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِّتَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ …﴿١٢﴾
12. Na Tumejaalia usiku na mchana kuwa ni Aayah (ishara) mbili. Basi Tukafuta Aayah ya usiku na Tukajaalia Aayah ya mchana kuwa ni ya mwangaza ili mtafute fadhila kutoka kwa Rabb wenu. [Al-Israa: 12]
Anasema pia:
وَجَعَلْنَا نَوْمَكُمْ سُبَاتًا ﴿٩﴾ وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا ﴿١٠﴾وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ﴿١١﴾
9. Na Tukafanya usingizi wenu mnono, mapumziko kama kufa. 10. Na Tukafanya usiku kuwa kama libasi la kufunika. 11. Na Tukafanya mchana kuwa ni wa kutafutia maisha. [An-Nabaa: 9-11].
v) Bin-Aadam ana khiari kutumia macho yake kutazamia anayoyapenda na asiyoyapenda. Mfano akitembea njiani akaona jambo baya linatendeka anaweza kujizuia asilitazame kwa kugeuza uso au kubadilisha njia. Ama masikio, hayana kizibo, kwa hiyo bin-Aadam hana khiari ila kusikia tu sauti inayomtokezea kwa ghafla.
vi)
Sikio ni linaposikia Qur-aan, humuathiri mtu na huenda ikawa ni sababu ya kuongoka kwake. Wapofotu watajilaumu Siku ya Qiyaamah pale watakaposema:
لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١٠﴾
Lau tungelikuwa tunasikiliza au tunatia akilini, tusingelikuwa katika watu wa motoni. [Al-Mulk: 10].
vii) Tumeamrishwa tuisikilize Qur-aan kwani huenda ikawa sababu ya uongofu kutokana na Rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:
وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾
204. Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa. [Al-A'araaf: 204].
viii) Kuhusu sababu ya kutajwa kusikia kwa upekee (singular) na kutajwa macho kwa wingi ni pale sauti kubwa ya ghafla inapotokea wakati watu wengi wamekaa mahali pamoja. Kisha kila mtu akasikia sauti ile ile moja ya aina yake; kama ni mpasuko, au sauti ya mnyama au ya sauti yoyote ile. Lakini macho ya kila mmoja yatakapoelekea kutafuta itokako sauti hizo, hayataangaza mahali pamoja. Kwa hiyo ingawa wote walisikia sauti ya aina moja, lakini kuangaza kwao kulitofautiana.
Na Allaah Anajua zaidi
…/2